Rais Xi aanza ziara ya kiserikali nchini Tajikistan

人民网

      (Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 05, 2024

      Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon akifanya hafla kubwa ya kumkaribisha Rais wa China Xi Jinping kwenye uwanja wa ndege wa Dushanbe, Tajikistan, Julai 4, 2024. (Xinhua/Yan Yan)

      DUSHANBE - Rais Xi Jinping wa China amewasili Dushanbe, Tajikistan siku ya Alhamisi usiku, akianza ziara yake ya kiserikali nchini humo baada ya kuhudhuria mkutano wa 24 wa Baraza la Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) mjini Astana, Kazakhstan.

      Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon amemkaribisha Rais Xi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dushanbe kwa hafla kubwa, ambapo vijana karibu 1,500 wa Tajikistan waliovalia mavazi ya kitamaduni walikuwa wakicheza ngoma na kupeperusha bendera za taifa za China na Tajikistan.

      Baada ya kuwasili, Rais Xi ameelezea matarajio yake kwa majadiliano kati yake na Rahmon kuandaa mipango mipya ya maendeleo ya uhusiano kati ya China na Tajikistan kwa kuzingatia hali mpya.

      Rais Xi amesema kutokana na juhudi za pamoja za nchi zote mbili, ziara yake hiyo inatarajiwa kuwa yenye mafanikio makubwa, na kuinua ushirikiano wa pande zote kati ya China na Tajikistan kwenye ngazi mpya.

      Ziara ya Rais Xi nchini Tajikistan itaongeza kasi na nguvu mpya katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi hizo mbili, Rais Rahmon aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua hivi karibuni.

      Rais Rahmon pia alisema uhusiano kati ya Tajikistan na China umeingia katika hatua mpya ya kihistoria, na kufungua matarajio mapya ya ushirikiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

      Miaka ya hivi karibuni wakuu hao wawili waliwasiliana mara kwa mara. Wakati wa ziara ya Rais Xi nchini Tajikistan Mwaka 2019, alitunukiwa Amri ya Taji kutoka kwa Rais Rahmon mjini Dushanbe. Nchi zote mbili zimeahidi kujenga jumuiya ya maendeleo na jumuiya ya usalama kati ya China na Tajikistan.

      Ziara ya Rais Xi, itatoa msukumo mpya kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na itatoa mchango kwa ustawi wa jumla wa Asia ya Kati, amesema Abdurakhim Juraev, profesa katika Chuo Kikuu cha Sheria, Biashara na Siasa cha Serikali ya Tajikistan mjini Khujand.

1/7