Rais wa Kenya awafukuza kazi mawaziri wa baraza baada ya wiki kadhaa za maandamano yenye ghasia

人民网

      (Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 12, 2024

      Picha hii iliyopigwa Julai 11, 2024 ikimuonyesha Rais wa Kenya William Ruto akitoa hotuba kwenye televisheni. (Xinhua/Dong Jianghui)

      NAIROBI - Rais William Ruto wa Kenya amewafuta kazi mawaziri karibu wote wa Baraza lake la Mawaziri siku ya Alhamisi kufuatia wiki tatu za maandamano dhidi ya serikali kupinga kuongezeka kwa ushuru ambapo wakati akihutubia mkutano na wanahabari jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, Ruto ametangaza kuwafuta kazi mawaziri 22 wa baraza hilo la mawaziri, akiwabakisha pekee naibu wake Rigathi Gachagua, na Kiongozi wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora Musalia Mudavadi.

      "Nimeamua kuwafuta kazi mara moja mawaziri na mwanasheria mkuu kutoka Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Kenya, isipokuwa kiongozi wa mawaziri ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje na diaspora," Ruto amesema.

      Amesema kuwa atashiriki katika mashauriano ya kina katika sekta tofauti na pande mbalimbali za kisiasa ili kuanzisha serikali yenye msingi mpana.

      Rais Ruto amesema hatua hiyo ni muhimu katika kushughulikia mzigo wa madeni, kuongeza rasilimali za nchini humo, kupanua fursa za ajira na kuondoa matumizi mabaya na mambo yasiyo ya lazima kwa majukumu yanayofanana ndani ya mashirika ya serikali.

      Amesema, katika kipindi hiki cha mpito, shughuli za serikali zitaendelea bila kukatizwa chini ya uongozi wa makatibu wakuu na maofisa wengine husika.

      Amesisitiza kuwa uamuzi huo umefanywa baada ya "kutafakari, kusikiliza Wakenya, na tathmini kikamilifu ya Baraza langu la Mawaziri."

      “Matukio yaliyotokea hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuondolewa bungeni kwa Mswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2024, yalikuwa mambo muhimu yaliyolazimu mabadiliko haya ya Baraza la Mawaziri,” Ruto amesema, akibainisha kuwa kuondoa mswada huo bungeni kunahitaji mapitio na upangaji upya wa bajeti na usimamizi wa fedha, ikifikisha serikali katika hatua ya mabadiliko.

      Mswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2024, ambao umezua maandamano makubwa, ulilenga kukusanya shilingi bilioni 346.7 (kama dola bilioni 2.7 za Kimarekani) zaidi kupitia ushuru mpya. Waandamanaji walikasirishwa sana na masharti ambayo yangeongeza ushuru kwa bidhaa na huduma muhimu, kama vile mkate na kutuma pesa kwa kutumia simu za mkononi.

      Kamisheni ya Taifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya inayofadhiliwa na serikali inasema kuwa, watu takriban 41 wameuawa na zaidi ya 360 kujeruhiwa katika maandamano hayo ya kupinga ongezeko hilo la ushuru nchini humo.

      Licha ya msukosuko huo, Ruto amesema serikali yake imepata mafanikio makubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kupunguza gharama ya pembejeo za kilimo, hivyo basi kupunguza gharama ya jumla ya chakula na maisha.

      Picha hii iliyopigwa Julai 11, 2024 ikimuonyesha Rais wa Kenya William Ruto akitoa hotuba mjini Nairobi, Kenya. (Joy Nabukews/Xinhua)

      (Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)