Maonyesho ya Teknolojia za Akili Mnemba Duniani kufanyika Tianjin, China

人民网

      (Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 13, 2024

      Mfanyakazi akichangamana na roboti kwenye Kongamano la tano la Teknolojia za Akili Mnemba Duniani katika Kituo cha Mikutano na Maonyesho cha Tianjin Meijiang, mjini Tianjin, Kaskazini mwa China, Mei 23, 2021. (Xinhua/Sun Fanyue)

      TIANJIN - Taarifa iliyotolewa kwenye mkutano na wanahabari siku ya Jumatano imesema, maonyesho ya Teknolojia za Akili Mnemba Duniani Mwaka 2024, yaliyopangwa kufanyika Tianjin, Kaskazini mwa China kuanzia Juni 20 hadi 23, yanalenga kujumuisha rasilimali zinazohusiana na teknolojia za Akili Mnemba (AI) nchini China na duniani kote.

      Maonyesho hayo yataandaliwa kwa pamoja na Mji wa Tianjin wa kaskazini mwa China na Mji wa Chongqing wa kusini-magharibi mwa China, yakijumuisha shughuli mbili ambazo zamani zilijulikana kama Kongamano la Teknolojia za Akili Mnemba Duniani huko Tianjin na Maonyesho ya Teknolojia za Kisasa ya China huko Chongqing.

      Shughuli hiyo ya AI inalenga kuunda jukwaa la kimataifa la uvumbuzi wa kitaaluma, maonyesho, mashindano na uhimizaji wa uwekezaji katika nyanja ya teknolojia za akili mnemba. Itavutia kampuni ongozi, taasisi mashuhuri za utafiti na vyuo vikuu bora.

      Ikichukua eneo la maonyesho lenye ukubwa wa mita za mraba 100,000, shughuli hiyo itajumuisha maeneo 10 ya maonyesho yenye mada zinazohusiana na AI, magari yaliyounganishwa na teknolojia za kisasa, uzalishaji bidhaa wa kutumia akili mnemba na roboti. Mashirika na taasisi kadhaa za kimataifa zitashiriki katika shughuli hiyo, zikishindana katika mambo ya roboti na changamoto za kuendesha gari kwa teknolojia za akili mnemba.

      Tianjin na Chongqing zote zimeongeza juhudi za kukuza mambo yao ya AI katika miaka ya hivi karibuni. Tianjin imeshuhudia mapato yatokanayo ya AI yakizidi yuan bilioni 300 (kama dola bilioni 41.4 za Kimarekani) Mwaka 2023. Na huko Chongqing, takwimu za serikali ya mji huo zimeonesha kuwa, viwanda vinavyohusiana na magari yaliyounganishwa na teknolojia za akili mnemba na magari yanayotumia nishati mpya vinafikia kwa kasi thamani ya matrilioni ya yuan.

      Miji hiyo mbili itapeana zamu kuandaa Maonesho ya Teknolojia za Akili Mnemba Duniani katika siku zijazo.

      (Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)