Mlinzi wa Kipepeo achunguza bioanuwai ya Yunnan, China

人民网

      (Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 12, 2024

      Vipepeo aina “Malkia wa mwitu” wakikusanyika kwenye kile kinachoitwa “Bonde la Vipepeo” huko Jinping, Mkoa wa Yunnan wa China. (Picha na Bai Meng/ China Daily)

      Yang Zhenwen ametumia miongo zaidi ya miwili akizunguka katika milima ya Kusini Magharibi mwa China akichunguza spishi mpya. Maisha yake yameingiliana sana na vipepeo, kiasi kwamba jamaa huyu mwenye umri wa miaka 47, amepewa majina matatu ya utani yanayohusu wadudu hao wenye mabawa.

      Akiwa mhifadhi wa Jumba la Makumbusho ya Kipepeo lililopo Wilaya ya Jinping, Mkoa wa Yunnan wa China, Yang mara nyingine huitwa “Baba wa Vipepeo” kwa sababu amezunguka milima ya mkoa huo kwa zaidi ya miongo miwili ili kuchunguza spishi mpya za vipepeo na kuchangia uhifadhi wao.

      Mkereketwa huyo wa vipepeo mwenye hamasa amekuwa akiambatana pamoja na wanasayansi kuizunguka milima ya Jinping, na hata kuchangia katika ugunduzi na utambuzi wa spishi mpya za vipepeo.

      Jumba lake la makumbusho ni maskani ya sampuli za vipepeo zaidi ya 2,200, na ni makao makuu ya Yang kueneza ujuzi kuhusu vipepeo na kuhimiza ufahamu wa watu kuhusu kulinda mazingira ya asili.

      Wakati anapotoa huduma ya kuongoza watalii katika makumbusho na wadau wa mazingira ya asili, Yang huwa “ensaiklopidia ya mambo ya vipepeo”. Na jina la “mlinzi wa vipepeo” amepewa pia Yang kutokana na kazi yake makini ya kulinda viumbe hao wadogo.

      Licha ya majina hayo mengi, Yang anajichukulia mwenyewe kama mtu wa kawaida tu. “Kama kuna kingine chochote, ninajifikiria mwenyewe kama mkereketwa wa vipepeo mwenye hamasa kwao ya kudumu” amesema Yang.

      Yang alizaliwa na kukulia katika mji mdogo wa Maandi huko Jinping. Mji huo una hali ya hewa nzuri yenye unyevunyevu, yenye halijoto ya wastani wa nyuzi 18 na mvua ya kutosha mwaka mzima. Kuna eneo la mianzi lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 2,670, ambalo huwapa vipepeo vyakula vya kutosha na mazingira bora ya kuzaliana.

      Tukio lisilo la kawaida hutokea huko Jinping kuanzia Mei hadi Juni kila mwaka, wakati ambapo vipepeo takriban milioni 100 huvunja via vya uzazi na kuruka nje kwenye wilaya hiyo yenye bioanuwai, ikitoa mandhari adimu inayojulikana kama “mlipuko wa vipepeo”.

      Utafiti unaonesha kuwa katika kile kinachoitwa Bonde la Vipepeo la Maandi kuna spishi zaidi ya 320 kutoka familia 11 za vipepeo kati ya familia zote 12 za vipepeo zinazopatikana nchini China.

      “Kwa sababu ni wadudu dhaifu sana, vipepeo pia wanaweza kuonekana kama alama ya afya ya ikolojia ya eneo husika, na ni katika mazingira tu yanayofaa na yenye afya, tukio la mlipuko wa vipepeo huweza kutokea,” amesema.

      Yang amesema kuwa takribani asilimia 90 ya vipepeo huliwa na wadudu wengine kabla ya kukua na kuwa wakubwa.” Matokeo yake, nyuma ya mlipuko huu wa vipepeo ni idadi kubwa ya wanyama mbalimbali. Vipepeo siyo tu hutoa mandhari ya kushangaza kwetu kutazama, bali pia huchangia kwenye bioanuwai,” ameongeza.

1/3